Jumatatu, 9 Septemba 2013

Maganga wa Iringa asema.....


Makala ifuatayo imeandikwa na Meshack Maganga- Iringa — Nilipoandika makala niliyoipa kichwa cha USIKUBALI KUWA MNYONGE WA KIUCHUMI NDANI YA NCHI YA TANZANIA, Nililezea jinsi ambavyo watanzania wanaweza kutumia fursa zilizopo kujiondoa kwenye umasikini wa kujitakia na pia kuacha tabia ya kulalamika sana bila kuchukua hatua. Katika makala ile, nilipata mwitikio mkubwa sana. Kwanza, nilipigiwa simu nyingi na kutumiwa barua pepe nyingi, baadhi ya wasomaji walifunga safari na kuja Iringa ili kujifunza kilimo cha miti, na baadhi yao waliamua kununua mashamba na wengine walinunua mashamba yenye miti kabisa.

Baadhi ya wasomaji walinitumia ‘meseji’ wakiuliza, ‘hayo unayo andika ni kweli unayafanya ama ni kilele tu?  Kuna mmoja wa wasomaji wa makala ile alinipigia simu na kusema wewe Maganga, umri wako na hayo unayoyafanya mbona haviendani?  Nilimjibu kwamba maendeleo hayafuati rangi ya mtu, umri, ama umbo, maendelea yaweza kwenda kwa mtu yoyote kama akiamini. Zaidi ya hayo niliwaomba  wote walionipigia, wakipata muda wanitembelee Iringa kujifunza kisha wachukue hatua.

Albert Sanga, ameandika makala yenye kichwa kisemacho KAMA UNA AKILI YA MATOPE; UTAKUWA NA MAISHA YA UDONGO amegusia wa kifupi sana jinsi ambavyo nilivyoanza kilimo cha mboga na miti kwa mtaji wa shilingi 25,000/ ninajua kwa mawazo ya kawaida ni vigumu sana hasa kwa wale walipopita  vyuoni na mashuleni kwa ujumla kuamini kile kinachosemwa, lakini ukweli ndio huo, niliweza kwa sababu kichwa changu kiliamini
kwamba ninaweza...sikuwa na muda wa kulalamika, wala kuilaumu serkali wama wazazi wangu. kwa sasa nimefanikiwa kukuza mtaji wangu na kununua mashamba yangu mengi sana unaweza kunitafafuta nikakupatia ushuhuda wangu.

Vifafa vya kiuchumi, ama kufulia husababishwa na mambo mengi sana, badhi ya sababu za vifafa vya kiuchumi ni pamoja na Kufanya mambo bila kufikiria na kupata ushauri wa kile unachotaka kukifanya iwe ni biashara ama ajira.Pia kuna wanao fahamu na wamezisikia fursa mbalimbali lakini bado wanasubiri muda ufike (waiting for the perfect moment) huenda wakaendelea kuusubiri muda muafaka mpaka watakapo zeeka.  Kuamini na kutegemea ajira pekee kwa kuiona ajira kama ndio muarobaini wa kutatua matatizo ya kiuchumi  pekee yake na kukaa bila kujishughulisha.

Nimeishi Iringa kwa muda wa miaka 9 sasa, nikiishi kwa kaka yangu ambae ni mjasiriamali wa kuigwa, wakati ule mwaka 2007 alikuwa akinifundisha uwekezaji kwenye aridhi na mashamba, kusema ukweli nilikuwa sielewi sana,  niliona ni kazi kubwa pia kushinda shambani ama kupanda miti kisha kuisubiri kwa miaka mitano ama saba, ninadhani sikumwelewa kaka yangu kwasababu nilikuwa na akili za ‘KICHUO’ chuoni nilikuwa nikipewa hela na ziliniweka kwenye black markets nikajisahau, nilipofika mwaka wa pili nilisoma kitabu maarufu duniani  kiitwacho ‘RICH DAD POOR DAD’ kitabu hiki kilinihamasisha sana na kubadilisha mtazamo wangu kuhusu maisha, ni mwaka huo nilipoanza kuwekeza kwa kununua shamba la ekari tano wilayani Mufindi, nilipomaliza chuo nikajikita zaidi katika kujifunza kutoka kwa kaka yangu Baraka, rafiki yangu Albert Sanga  na Rich Dad wangu wa Mafinga ambae ni mwenyekiti wa wapanda miti mkoa wa Iringa. Msomaji atakae penda kujua zaidi nipo wapi kwa sasa anitafute.

Kuna wale ambao wameamua kuitegemea serikali kabisa kwa kila kitu, wanaamka asubuhi, wanaoga, wanapata kifungua kinywa, wanaelekea vijiweni kucheza karata na kucheza ‘pool’ asubuhi mapema bila kuwajibika, hawazalishi matokeo yake ni vifafa vya kiuchumi.

Kuufikia mafanikio  si rahisi kutokana na nguvu za nje zinazoweza kukufanya usahau haya kama uvivu, ujinga, kutosikiliza ushauri kwa waliofanikiwa, kutokuwa na mshauri (mentor) anayefanya yale unayotaka kuyafanya, uoga, kutojifunza mambo mapya, kuwa na marafiki wanaosema ponda mali kufa kwaja, kupokea ushauri wa ‘bure’ kutoka kwa ndugu na marafiki ambao wanaamini kwamba ujasiriamali ni kipaji na kwamba ni kazi ya waarabu, wahindi, wachaga, wakinga ama wazungu peke yao.

Na kama bado una imani kwamba ni wajibu wa serikali, mbunge wako maarufu, au kiongozi wako maarufu wa chama cha siasa ukipendacho ambacho unakipigania usiku na mchana, mpaka unakosa muda wa kufanya mambo yako binafsi au kama umeweka mawazo kichwani kwako kwamba, mabadiliko ya katiba mpya yatasaidia kufulia kwako,utakuwa unapoteza muda wako, na kwa hakika utakuwa unavikaribisha vifafa vya kiuchumi maishani mwako.

Au, kuwa na  watu lukuki na watumiaji wa mali zako nyuma yako (people behind you) na utamaduni wa kuyachukulia mambo kama yalivyo kana kwamba ni utaratibu tu au utamaduni wa bora liende ili mradi kumekucha na hasa ukosefu wa nidhamu katika maisha wa kufikiria siku kwa siku au wiki kwa wiki ( thinking day to day or week to week).

Usije ukashangaa siku ya mwisho wa dunia unaulizwa na Mungu, swali kama hili, ulitumiaje muda na rasilimali watu na  kipawa chako kwa muda wote wa  wamaisha yako ulipokuwa Tanzania? utajibu nini? utakata rufaa au utatafuta wakili wa kukutetea? Fikilia chukua hatua za kuanza kuwekeza taratibu.

Kumbuka kuwa haukuletwa duniani kulala,kushabikia mambo yasiyokuwa na maana, au yasiyokuhusu, au kuwa mwanaharakati wa harakati zisizokuwa na kichwa wala miguu, au kutuwama kama maji machafu shimoni.Au kuishi maisha ya ujanja wa mbuni wa kuficha kichwa chake kwenye mchanga huku kiwiliwili kikiwa nje. Wewe ni kiumbe cha pekee kinachotakiwa kubadilika kila siku kimwili, kiakili, kifikra, kiuchumi, kiutamaduni, kiroho  na hata kiuongozi wa biashara yako.

Kila jambo linalokutokea kama mjasirimali au mtu wa kawaida  ni matokeo ya uchaguzi wako wa awali. Angalia mfano huu, tukio (event) unapata shilingi 250,000/, uamuzi wako (response) unazitumia hizo hela kwenye vilabu maarufu unavyovifahamu kwa kuwafurahisha watu wako(people behind you), matokeo ya uamuzi wako  (outcome) unaishi maisha ya ‘tafadhali nipigie’ na kuendelea kulaumu watu wasiopaswa kulaumiwa hasa serikali.

Mfano wa pili ni kinyume cha huo hapo juu. Tukio (event) unapata shilingi 250,000/, uamuzi wako (response) unawekeza  hizo hela kufungua mradi mdogo ama kwa kulipia semina za ujasiriamali,  na kununua vitabu vya kujifunza ama kwa kusomesha mtoto wako, matokeo ya uamuzi wako  (outcome) unakuwa umeandaa ndoto yako na hautaishi kwa kuisubiri serikali au kiongozi wako.Unaondokana na vifafa vya kiuchumi. Unajua aina ya watu anaoshinda nao mtu anapokuwa na fedha inaamua sana aina ya maamuzi anayoyafanya katika fedha aliyoshika

Kwa kuhitimisha, bado nitaendelea kutoa muda wangu kwa mtu atakae hitaji kuwekeza kwenye kilimo cha miti, na mashamba ya kuuza bado yapo, nitakusaidia kama mimi nilivyo saidiwa na watu wengine. “USIKUBALI KUWA MNYONGE WA KIUCHUMI NDANI YA TANZANIA.

meshackmaganga@gmail.com 


Source: http://www.wavuti.com/4/post/2013/09/meshack-ukizoea-kulalamika-kunungunika-unakaribisha-vifafa-kiuchumi.html#ixzz2eRc5U0Ap

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni