Jumapili, 21 Julai 2013

Usiache kuisaidia serikali yetu ukiwa mtaani


 
Picture
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM

Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz
Julai 20, 2013

ILI kuboresha utoaji huduma kwa umma hivi karibuni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeanzisha utaratibu wa kupokea malalamiko na taarifa kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani.

Utaratibu huu mpya unatarajia kupunguza usumbufu na gharama kwa walalamikaji, hususan watokao pembezoni mwa nchi katika kuwasilisha malalamiko yao ofisi za Tume na kupata mrejesho. Itakumbukwa kuwa hapo awali baadhi ya wananchi walilazimika kuacha shughuli zao za kiuchumi na kusafiri hadi zilipo ofisi za Tume ili kupata huduma.

Vilevile utaratibu huu utaharakisha mawasiliano kati ya Tume na walalamikaji kwa upande mmoja na kati ya Tume na walalamikiwa, ukilinganisha na njia iliyokuwa ikitumika awali ya barua ya posta ambayo ilikuwa ikichukua muda mrefu na kukabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo kupotea kwa barua na wananchi wengi kutokuwa na anuani za posta za uhakika.

Kwa utaratibu huu mpya mtu anaweza kufungua malalamiko Tume pale ambapo ataona haki zake za msingi 
zimevunjwa au misingi ya utawala bora imekiukwa kwa kuandika ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani kwenda namba 0754 460 259, naye atapokea majibu ndani ya muda mfupi.

Utaratibu huu mpya siyo tu unampa uhakika mlalamikaji wa lalamiko lake kufika Tume, bali pia unamwezesha kupata ushauri wa kisheria juu ya lalamiko lake ndani ya muda mfupi.

Aidha, utaratibu huu utaisaidia Tume kupata vidokezo (yaani ‘tips’) kuhusu matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora yanayotokea maeneo mbalimbali ya nchi na hivyo kufanya ufuatiliaji kwa wakati.

Utaratibu huu mpya unatarajia kuongeza idadi ya malalamiko yanayowasilishwa Tume kutoka wastani wa malalamiko 80 hivi sasa hadi 200 kwa Mwezi. Tume imejipanga kikamilifu kuyashughulikia malalamiko yote ndani ya muda mfupi. Hii inatokana na ukweli kwamba hivi sasa Tume inatumia mfumo wa kielektroniki ujulikanao kwa lugha ya kigeni kama “Case Management System,”  katika kushughulikia malalamiko yanayopokelewa.

Tunaomba vyombo vya habari vitusaidie katika kuhakikisha utaratibu huu mpya unafahamika vizuri kwa umma na kuwahamasisha wananchi wautumie kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu masuala ya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Jinsi ya kuwasilisha lalamiko kwa simu ya kiganjani:
·         Tuma lalamiko lako ukianzia na neno 'REPORT' kwenda Na0754 460 259. Mfano: REPORT shule ya Msingi Kwetumbali, DSM tunachapwa viboko zaidi ya kumi.

·         Utapokea ujumbe usemao lalamiko lako limepokelewa Tume, na utaelekezwa kama unayo maelezo zaidi yatume kupitia barua pepe: chragg@chragg.go.tz au simu Na. 22 2135747/8.

·         Maafisa wa Tume wanaweza kukupigia simu ili kupata maelezo zaidi kabla ya kuanza kushughulikia lalamiko lako.

·         Lalamiko lako litakapoanza kushughulikiwa, utapata ujumbe wa simu kukujulisha Namba  ambayo utaitumia kufuatilia lalamiko lako. Namba hii itatumwa kwako kupitia namba ya simu uliyotumia kuwasilisha lalamiko lako.

·         Utaweza kujua hatua ambazo maafisa wa Tume wamefikia kwa kutuma ujumbe wa simu pamoja na Namba ambayo utakuwa umepewa baada ya lalamiko lako kufunguliwa jalada.

Jinsi ya kufuatilia lalamiko lako:
·         Tuma ujumbe wako ukianza na neno 'STATUS' kwenda Na.0754 460 259. Mfano: STATUS 13024.

Utaratibu huu wa upokeaji wa taarifa na malalamiko kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani umefadhiliwa na Programu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa nchi zinazoendelea (SPIDER) ya nchini Sweeden (au Swedish Program for ICT in Developing Regions).

Tunaomba ieleweke kuwa utaratibu huu mpya haubadilishi taratibu zilizokuwa zikitumika awali za kuwasilisha malalamiko Tume. Sambamba na uwasilishaji wa malalamiko kwa ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani, Tume itaendelea kupokea malalamiko ya wananchi kwa mlalamikaji kuja mwenyewe kwenye ofisi zetu na kufungua lalamiko lake, na kwa kuandika na kutuma barua kwa njia ya posta, barua pepe au nukushi (faksi.

THBUB ni taasisi huru ya Serikali iliyoanzishwa kama taasisi ya kitaifa iliyo kitovu cha kukuza na kulinda haki za binadamu na wajibu na misingi ya utawala bora.  Ilianzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 chini ya Ibara ya 129 (1) na Sheria Na. 7 ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Mwaka 2001 na ilianza kazi rasmi tarehe 1 Julai, 2001.

Tume ina majukumu mengi, baadhi ya majukumu hayo ni:  Kupokea na kuchunguza malalamiko yanayohusu uvunjwaji wa haki  za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na kutoa mapendekezo, kufanya utafiti na kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya haki za binadamu na utawala bora, na kutoa mapendekezo kwa ajili ya kuboresha sheria na kanuni zilizopo au miswada ya sheria na kanuni au taratibu za kiutawala ili kuhakikisha kuwa haki za binadamu na utawala bora vinazingatiwa.

Tume inafanya kazi Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar. Kwa hivi sasa ina ofisi nne (4) zilizoko Dar es Salaam, Zanzibar, Lindi na Mwanza.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Afisa Uchunguzi Mkuu, Bwana Germanus Joseph
Simu: +255 22 2135222/ 754 768 346.

Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa,
Bwana Wilfred Warioba
Simu: +255 22 2135747/8; 714 818 177.


Source: http://www.wavuti.com/4/post/2013/07/simu-email-za-kutuma-malalamiko-kwa-tume-ya-haki-za-binadamu-na-utawala-bora.html#ixzz2ZjpKLzzn

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni